Jumanne, Aprili 29, 2014

 RAIS Jakaya Kikwete, ametoa msamaha kwa wafungwa 3,967 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho miaka 50 ya Muungano wa Tanzania. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, Rais ametoa msamaha kwa wafungwa kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya ibara ya 45 (1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia Rais Kikwete amepunguzia wafungwa wote moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49 (1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(1-xviii).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo wafungwa watakaopata msamaha huo ni wale wenye magonjwa ya Ukimwi, kifua kikuu na kansa, wazee kuanzia umri wa miaka 70 na zaidi ambao wamethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya.

 Alisema wafungwa wengine ni wale wenye ulemavu wa mwili na akili ambao pia wamethibitishwa na jopo la waganga chini Uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya wakiwemo pia wafungwa wanawake walioingia na ujauzito gerezani na wale wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya walioingia nao gerezani.

Msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa,wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani,wafungwa wa kupokea na kutoa rushwa,unyang'anyi na unyang'anyi wa kutumia silaha,wafungwa waliopatikana na silaha au risasi. Wengi ambao hawahusiki na msamaha huo ni wafungwa wanaotumikia vifungo kwa kulawiti,kunajisi na kubaka.

 "Mbali na wafungwa hao, lakini wengine ni wale waliohukumiwa adhabu ya kifo na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani na wale wote waliofungwa kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya," alisema Chikawe.

Chikawe aliongeza kuwa, wafungwa wengine ambao hawahusiki na msamaha huo ni wale waliofungwa kwa makosa ya wizi wa magari kwa kutumia silaha,waliotoroka au waliojaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali ambao wanatumikia kifungo hicho gerezani na wale waliopatikana na hatia kwa kutumia madaraka yao vibaya.

Aliwataja wengi kuwa ni wafungwa wanaotumikia kifungo kwa kosa la kufanya biashara haramu ya binadamu,nyara za Serikali,ubadhirifu wa fedha za Serikali. Wengine ni wafungwa waliopata msamaha na Rais ambao bado wapo gerezani kutumia sehemu ya kifungo kilichobaki.

 Wengine ambao wataendelea kutumikia adhabu zao ni wale waliofungwa kwa kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea, wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya sheria ya Bodi ya Parole (Act. No.25/1994) na sheria ya Huduma kwa Jamii (Act.No.6/2002. )

Kundi la Mwisho ambalo halitahusika na msamaha huo ni wale waliopata msamaha wa 1/6 ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la Kawaida lililotolewa chini ya kifungu cha 49(1) cha sheria ya Magereza sura ya 58 na bado wafungwa hao wanatumikia kifungo kilichobaki.

0 comments:

Chapisha Maoni