Jumatano, Februari 05, 2014

Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Majaliwa Kassim Majaliwa ameanzisha  vilabu  102 vya  michezo kwa kuvipatia jezi na mipira ili kuhakikisha vijana wa jimbo hilo lililopo mkoani Lindi hawajishughulishi na matukio ya uhalifu .

Majaliwa ambaye pia ni Naibu waziri wa Elimu TAMISEMI aliyasema hayo hivi karibuni  wakati wa kilele za sherehe za kutimiza miaka 37 ya  Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika katika kata ya  Likunja wilayani humo.

Katika sherehe hizo Mbunge huyo alizipatia timu za mpira wa miguu za Uhuru City na Mbagala City jezi seti  moja kwa kila timu na mpira mmoja ambapo timu hizo zilipanda uwanjani na kuchuana yote hiyo ikiwa ni kusherehekea  CCM kutimiza miaka 37 .

Baada ya kumalizika kwa mashindano hayo timu ya Uhuru City iliibuka  mshindi wa mabao mawili kwa nunge  dhidi ya timu ya Mbagala City.

Naibu waziri Majaliwa pia  ameviwezesha vikundi mbalimbali vya ngoma  katika wilaya hiyo ambavyo vinajipatia  pesa kwa ajili ya kazi ya sanaa na kuweza kujikwamua kiuchumi.

Sherehe hizo zilienda sambamba na maandamano ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi na kupambwa na burudani ya  ngoma za asili, kwaya na mziki kutoka kwa wasanii mbalimbali kikiwemo kikundi cha Wanapakaya kutoka wilayani Kilwa na msanii Dogo Doto.

0 comments:

Chapisha Maoni