Alhamisi, Februari 06, 2014

Shaggy Sadick mwenye umri wa miaka 18, mkazi wa Musoma mjini Mkoa wa Mara.

MATESO kila kukicha. Kijana Shaggy Sadick mwenye umri wa miaka 18, mkazi wa Musoma mjini, Mkoa wa Mara yuko katika mateso makubwa baada ya tumbo lake kuvimba na kuongezeka ukubwa hali inayomfanya ashindwe kutembea.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa, dada wa Shaggy, Mariam Sadick, alisema mdogo wake alianza kuumwa ugonjwa huo tokea akiwa na umri wa miaka 12 na kwa muda wote huo, wamehangaika katika hospitali mbalimbali nchini bila mafanikio.

Alisema awali walianza kumpeleka katika Hospitali ya Musoma na baadaye Bugando jijini Mwanza ambako baada ya vipimo, iligundulika kwamba alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo ambao umejaa maji, ugonjwa ambao anapaswa kutibiwa nje ya nchi ili kuumaliza.

“Kwa kweli tumehangaika naye sana kumsaidia apone, lakini imeshindikana kwani ili apone, wanapaswa kumpeleka nje ya nchi kwa matibabu, kitu kinachotishia uhai wake kwani familia ni duni,” alisema dada huyo.

Dada huyo alizidi kulia kwa kusema kwamba kingine kinachomsikitisha ni kwamba mdogo wake amekosa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu kwani kwa matatizo aliyonayo, hawezi kutembea tumbo limefika hadi magotini.

Alisema wakati wa kulala ukifika, mdogo wake hupata wakati mgumu kwani wanalazimika kumuwekea mito mingi ya kulalia nyuma yake, vinginevyo anaweza kupoteza maisha kwa sababu ya kushindwa kupumua vizuri.

“Kwa kweli kitu ambacho kinatusikitisha wote ni kukosa kufanya mtihani wa kidato cha nne, maana hawezi kutembea tena  wakati wa kulala ndiyo kama hivyo,” alisema.

 Mtoto Shaggy yupo katika mateso makali sana, anahitaji msaada wa hali na mali ili aweze kuyaokoa maisha yake ili apate matibabu, endapo utaguswa na habari yake, wasiliana na chumba cha habari kwa namba  0713 612 533.

0 comments:

Chapisha Maoni