Jumamosi, Aprili 05, 2014

WANANCHI  wenye  hasira  kali wakazi  wa  mtaa wa Mtwivila D katika Manispaa ya  Iringa wamemuua mtuhumiwa mwingine wa ujambazi  aliyetambulika kwa  jina la Ayubu Mhema (31) msukuma mkokoteni mkazi wa  Wangama mkoani Njombe  kwa tuhuma  za wizi  wa  mali za  wananchi  wa  eneo  hilo.

Tukio  hilo   lilitokea leo  majira ya saa 3  asubuhi baada ya  mtuhumiwa  huyo  kukamatwa akiwa na nguo zilizojaa gunia  moja ambazo  aliziiba katika   nyumba ya  mkazi  mmoja wa  eneo  hilo  baada ya  kuvunja mlango. 

 Hapa  mwili wa mtuhumiwa  huyo ukishushwa  kwa ajili ya kuhifadhiwa  chumba cha maiti  Hospitali ya  rufaa ya mkoa  wa Iringa.

 Mtuhumiwa wa  wizi Ayubu Mhema akiwa amelala  hoi.

Wakizungumza na  mwandishi  wa  habari hizi pasipo  kutaja majina  yao  wananchi hao  walisema  kuwa  kumekuwepo na matukio  endelevu ya  wizi katika  eneo hilo na  mbali ya  wezi  hao kukamatwa na kufikishwa  polisi  ila  bado  wamekuwa  wakiachiwa  huru jambo ambalo  limeongeza wimbi la wizi  katika  eneo  hilo.

Hata  hivyo  walisema mtuhumiwa  huyo Mhema amepatwa  kukamatwa eneo  hilo zaidi ya mara nne  akiwa na  wenzake ila  mbali ya  kupewa  kichapo bado  amekuwa akirudia  kuiba .

Mbali ya  kulalamikia  matukio  hayo ya  wizi  yanayoendelea katika  eneo hilo bado  waliwatuhumu  viongozi  wa serikali ya mtaa  kwa  kushindwa  kuitisha  mkutano  wa dharula kwa ajili ya  wananchi  kupiga   kura ya siri kwa lengo la kuwataja watu  ambao  wamekuwa  wakijihusisha na mtandao  wa  wizi  na  wale  wanaofunga mtandao huo ambao  baadhi yao  wanadaiwa ni  viongozi  wa mtaa huo.

" Tumekuwa  tukiomba kufanyika kwa mkutano na kila  wiki  mtendaji na mwenyekiti  wamekuwa  wakisogeza mbele  mkutano  huo huku  wananchi  tukiendelea kunyanyasika na mtandao  huo  wa  wezi ....ila tunasubiri kwa mara nyingine  mkutano wa April 27  kama  walivyotangaza na iwapo  watashindwa  tutapambana na viongozi hawa kwa  kumkataa mtendaji wa mtaa na kata  pamoja na  wajumbe  wake wote "

Kwani  walisema katika mkutano wa mwisho uliofanyika mwezi  uliopita  mbele ya  diwani wa kata ya Mtwivila Vitus Mushi  wananchi kwa kauli  moja  waliomba mkutano  huo ila viongozi  hao  wamekuwa  wakimpuuza hadi  diwani wao kwa  kushindwa  kusikiliza  maombi ya  wananchi .

Pia  walisema orodha  kamli ya majina ya mtandao  huo  wa  wezi  ilitajwa  na mtuhumiwa  huyo Mhema kabla ya  kufariki  ambapo mtandao huo upo  stendi ya Mlandege ,stendi kuu , Ilala kwa Mlyuka pamoja na Kihesa ambako  ndiko  yupo mmiliki wa mtandao  huo ambapo majina  yao  yamehifadhiwa .

Mwandishi wa habari  hizi alishuhudia polisi  wakifika  eneo hilo wakiwa na mabomu ya machozi kwa ajili ya kumuokoa  mtuhumiwa  huyo na kumchukua kumkimbiza  Hospital ya  Rufaa ya mkoa  wa Iringa kabla ya kufariki  dunia  njiani .

Ndani ya  wiki  hii  moja  wananchi  hao  wa mtaa wa Mtwivila D  wamewatesa  hadi  kufa  watu  wawili kwa  tuhuma  za wizi ambapo  jeshi la polisi  limewaonya  wananchi hao  kuacha tabia ya  kujichukulia  sheria  mkononi  dhidi ya  watuhumiwa  wa  wizi  na kuwa kufanya  hivyo  ni kosa na ni kinyume na haki  za binadamu.

0 comments:

Chapisha Maoni