Alhamisi, Aprili 03, 2014

Dk Margareth Zziwa.

Wabunge 33  wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wamesema mchakato wa kumng'oa madarakani  Spika wa Bunge hilo, Dk Margareth Zziwa uko pale pale.

Wamesema watatoa taarifa kwa marais wa Jumuiya ya Afrika (EAC) wa  nchi tano juu ya mambo mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni wa spika huyo.

Akisoma tamko mjini hapa jana,  kwa niaba ya wabunge hao wanaounga mkono hoja ya kumng'oa Zziwa,  Aballah Mwinyi ambaye ni  mbunge wa Tanzania, alisema juzi spika alikiuka sheria na kanuni.

Alisema alikiuka kanuni za kuongoza Bunge saa 8:30 alasiri kwa kuingia saa 10:00 alasiri.
Aidha, alitakiwa kutoingia kwa kofia ya uspika, badala yake, Katibu wa Bunge hilo, Kenneth Madete ndiye aliyepaswa kuliongoza na sababu ni kwamba kulikuwa na hoja ya wabunge kutokuwa na imani naye.

Wabunge hao walidai wanawasiliana na Madete na Mwanasheria wa Afrika Mashariki, Wilbard Kahwa  kupitia Kifungu cha sheria  namba 56 (b) cha Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), waweze kumng'oa madarakani.

Juhudi za waandishi wa habari kumpata Zziwa kutoa ufafanuzi wa mgogoro huo, hazikufanikiwa baada ya wasaidizi wake kusema ameahidi kuwatumia maelezo kwenye barua pepe.

Spika huyo aliahirisha bunge la EALA juzi kwa muda usiojulikana. Alifanya hivyo baada ya kuwepo mabishano, yanayohusu mkakati wa baadhi ya wabunge kumng'oa, wakidai ameshindwa kufanya kazi kwa viwango. Anatuhumiwa kufanya upendeleo miongoni mwa wabunge.

0 comments:

Chapisha Maoni