Alhamisi, Aprili 03, 2014

Mkazi wa Kijitonyama, Cresence Nguzo (25) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kujaribu kumuua askari wa kikosi cha usalama barabarani.

Nguzo alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Gabrieri Mirumbe.

Wakili  Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka alidai kuwa, Machi 23 mwaka huu katika makutano ya barabara za Bibi titi na Ali Hassan Mwinyi, Nguzo alijaribu kumuua askari Kostebo John kwa kumgonga na gari.

Mshitakiwa alikana mashitaka na  kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, kesi itatajwa tena Aprili 16 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Mwanasheria wa kujitegemea, Felix Mkongwa alifikishwa katika mahakama hiyo akikabiliwa na mashitaka ya kughushi na kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.

Wakili wa Kweka alidai mbele ya Hakimu  Mkazi Aloyce Katemana kuwa, Januari 3 mwaka  2005, Mkongwa alighushi hati ya makubaliano ya kubadilisha umiliki wa kiwanja namba 600 block G kilichopo Tegeta, akidai imesainiwa na George Kiwaga ambaye ni mmiliki jambo ambalo si kweli. Alikana mashitaka.

0 comments:

Chapisha Maoni