Jumatano, Februari 05, 2014



WANAFUNZI wa shule ya msingi na sekondari ya St Anne Marie Academy ya Dar es Salaam, wamefanya vurugu zilizoambatana na uharibifu mkubwa wa mali ikiwamo kuvunja vioo vya magari, mabweni, madarasa na kompyuta, chanzo kikidaiwa kuwa ni hatua ya uongozi wa shule kuwapa walinzi mamlaka makubwa ya kuwaadhibu.Mamlaka hayo walidai yameendelea kujidhihirisha kwa muda mrefu ambapo usiku wa kuamkia jana, mwanafunzi Loshilaa Emmanuel wa kidato cha sita, alipigwa na mlinzi na kushonwa nyuzi kadhaa, jambo lililosababisha wanafunzi wa bweni kuamka na kufanya vurugu za kuharibu mali baada ya kumkosa mlinzi aliyedaiwa kumpiga mwenzao.Vurugu hizo zinadaiwa kufanywa katika kipindi cha saa moja, kati ya saa nane usiku na saa 10 alfajiri jana na tayari Polisi Mkoa wa Kinondoni inashikilia wanafunzi tisa wanaodaiwa kuwa vinara wa vurugu hizo.

Wanane kati yao ni wa kidato cha sita na mmoja ni wa kidato cha nne. Mali zilizoharibiwa ambazo blog hii pamoja na kuelezwa, lilizishuhudia shuleni hapo ni pamoja na kuvunjwa vioo vya magari 17 ya shule, madirisha, taa na milango ya mbao katika madarasa yote hasa ya sekondari na ofisi, kompyuta 40 kuharibiwa huku nyingine 16 mpya za mpakato zikiibwa.

Viongozi wa wanafunzi waliozungumza na blog hii shuleni hapo jana, kwa nyakati tofauti walilaani vurugu hizo na kudai kuwa, lawama hazipaswi kuishia kwa wanafunzi pekee hata kama wamefanya kosa kisheriam kwa kuwa tukio hilo linahusisha malalamiko ya muda mrefu ambayo hayajashughulikiwa yaliyojenga uhasama baina ya walinzi wa shule, uongozi wa walimu na wanafunzi.

Miongoni mwa malalamiko ni pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari, Mary Msangi kuwapa mamlaka walinzi wa shule hiyo yenye wanafunzi wa kutwa na bweni kuanzia chekechea hadi kidato cha sita, kupiga wanafunzi wa sekondari kipigo chochote wanapokosa kutii sheria za shule.

“Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya wanafunzi kuhusu hawa maafande (walinzi) wetu, usiku wanapokea hongo na kuruhusu wanafunzi watoke huku wengine wakiwazuia, wengine wanaingiza vitu mpaka vileo, lakini wengine wakitaka kutoka kunazuka ugomvi, ni kama wana njaa kali, sasa kuna adhabu wanatoa zilizopitiliza ikiwamo vipigo,” alisema kiranja mkuu wa kiume wa kidato cha sita, Innocent Mwombeki.

Kiranja mkuu wa kiume wa kidato cha kwanza hadi cha nne, Hassan Haruni alisema kuna matukio ya kupigwa wanafunzi hata kwa makosa ya kurekebishwa pekee bila adhabu na kueleza kuwa, kabla ya tukio la jana, wanafunzi zaidi ya wanne walishapigwa na walinzi.

“Mambo yanakuwa mabaya zaidi kwa kuwa baadhi ya walimu viongozi wanahusika, kwa mfano hivi karibuni Mkuu wa Shule (Msangi) alitangaza katika mkusanyiko wa shule, kwamba amewapa mamlaka askari wapige wanafunzi ila wamwachie roho,” alisema Emma Mhagama, kiranja mkuu wa kike wa kidato cha kwanza hadi cha nne.

Mkuu wa Shule Kiongozi Mkuu wa Shule Kiongozi, Johanssan Rwebugisa aliliambia blog hii ofisini kwake kuwa, ni mapema kuthibitisha madai hayo kwa kuwa mengi yalishashughulikiwa ingawa alikiri kuwa tukio la mwanafunzi kupigwa na mlinzi usiku wa kuamkia jana haliwezi kuwafanya wanafunzi washambulie shule nzima na kuharibu mali kama walivyofanya.

“Siwezi kuwa na maelezo mengi, ila hii inaonekana kuwa ni jambo la muda linalohitaji uchunguzi, hatutajua sababu hasa, kwa kuwa kama ni malalamiko kuna utaratibu wa kuyawasilisha na kushughulikiwa na hawajawahi kuyaleta kwangu, labda walipeleka kwa Mkuu wa Shule,” alisema Rwebugisa.

Akielezea kilichotokea, Rwebugisa alisema wanafunzi wa bweni, wengi wao wakiwa kidato cha sita, walifanya vurugu baada ya kupata taarifa kwamba mwanafunzi mwenzao aliyekuwa akijisomea, kapigwa na mlinzi.

Mwombeki alisema hana uhakika kama ni kidato cha sita pekee walihusika na vurugu, kwa kuwa saa nane usiku waliamshwa na wenzao kwenda kumsaidia aliyejeruhiwa na mlinzi baada ya kupishana kauli, na wakiwa zahanati ya shule, wanafunzi wa bweni wa vidato vya chini waliamka na kufanya vurugu wakati wao wakiwa zahanati na mwenzao.

“Inaelezwa Loshilaa alitaka kutoka nje, mlinzi akamzuia, wakaanza kubishana, ndipo mlinzi akachukua shoka, upande wa mpini akampiga nao, tuliposikia tuliamka ilikuwa saa nane usiku hivi, tukampeleka hospitali tukiwa wengi kiasi, tulikaa nje kumsubiri, wazazi wake walipofika wakamchukua na kumpeleka Kituo cha Afya cha Bochi, Kwa Musuguri, ndipo wengine wakaamka na kuanza kuvunja mali,” alieleza Mwombeki.

Kiranja wa kike wa Kidato cha Sita, Lidya Mkumbo alisema katika bweni la wasichana la kidato cha sita, walishuhudia wanafunzi wa kiume waliokuwa wamevaa kaptula bila mashati wakirusha mawe kwenye bweni lao na kuvunja taa ndipo mwalimu mlezi alipowaamuru waingie ndani na kuwafungia mlango kwa nje hadi saa moja asubuhi.

Mkumbo alisema awali walitoka baada ya kuelezwa kuwa mlinzi anapigwa huku baadhi ya wanafunzi wakidai kama ni mlinzi anapigwa ni bora aendelee kupigwa, kwa kuwa hakukuwa na uhusiano mzuri kwa muda mrefu baina ya walinzi na wanafunzi.

Mkuu wa Wilaya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alitembelea shuleni hapo jana akifuatana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura na kuagiza chanzo kitafutwe na uchunguzi zaidi ufanywe, huku akielezea wasiwasi wake kuwa tukio hilo huenda likahusisha pia ushawishi wa walimu kutokana na uharibifu uliofanywa na wanafunzi.

“Siamini kama mwanafunzi mmoja kupigwa na mlinzi, adhabu inaweza kuwa ni uharibifu huu wa mali, ingeingia akilini kama tungesikia mlinzi kajeruhiwa baada ya kushambuliwa na wanafunzi kwa kumpiga mwenzao, ingawa nalo ni kosa kisheria, lakini kuna mantiki kuliko la kushambulia mali za shule namna hii, iko wapi nidhamu ya elimu?” Alihoji Rugimbana.

Alisema kama mwekezaji wa shule hiyo akiamua kufunga mradi huo na kufungua mwingine, hasara ni kwa Taifa, kutokana na mchango mkubwa wa sekta binafsi katika elimu, hivyo alisisitiza wanafunzi kuheshimu maadili na thamani kubwa ya ada wanayolipiwa na wazazi ama walezi wao kupata elimu hiyo.

Ada kwa sekondari katika shule hiyo inakaribia Sh milioni mbili kwa mwaka. Kamanda Wambura alisema polisi imeimarisha ulinzi eneo hilo hasa kutokana na kuwapo kwa wanafunzi watoto wa chekechea na shule ya msingi ambao vurugu kama hizo huwaathiri zaidi zikitokea na kwamba wanaendelea kuchunguza chanzo hasa cha tukio pamoja na thamani ya uharibifu wa mali.

Alitaja wanafunzi waliokamatwa kuwa ni Marko Mkemi, Mandela Soka, Fabran Fulena, Stanford Shomiki, Mwombeki Abdoni, Anyengise Frank, Amandus Kimano, Godfrey Ndimila wote wa kidato cha sita na Emmanuel Mtesha wa kidato cha nne. Msangi alipoulizwa kuhusu madai ya uongozi wa shule kuwapa mamlaka walinzi ya kupiga wanafunzi, alisema msemaji pekee wa shule kwa sasa ni Mkuu wa Shule Kiongozi ingawa alidai walinzi hao hawana mamlaka hayo.

Mmiliki wa Shule hiyo, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza akizungumza na blog hii kwa simu jana, alisema ameshtushwa na tukio hilo lakini hawezi kueleza chochote kwa kuwa hajui chanzo na kuwa leo, kutakuwa na mkutano wa dharura wa Bodi ya Shule, kuzungumzia suala hilo na hatua za kuchukua.

0 comments:

Chapisha Maoni