Jumamosi, Februari 08, 2014

Mtoto mchanga wa umri wa wiki mbili, ameuawa kwa kunyongwa shingo na baba yake mzazi, katika ugomvi wa kifamilia, uliotokea katika Kijiji cha Ibamba, wilayani Bukombe, katika Mkoa wa Geita.

Mtuhumiwa wa mauaji hayo ni kijana mfanyabiashara wa umri wa miaka 28 ambaye  inasemekana amekuwa katika mgogoro na mke wake, Juliana Juma (20) tangu alipotoka mahabusu huko Biharamulo.

Habari zilisema mtuhumiwa huyo alikuwa anashikiliwa kwa tuhuma za  kuiba mifugo.

“Alipotoka mahabusu mwaka jana, alikuta mke wake akiwa na ujauzito na baada ya kujifungua, mwanaume alidai kwamba mtoto si wake,” kilisema chanzo chetu cha habari.

 Kamanda wa polisi mkoani Geita, Leonard Paulo, alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku.

Alisema mtu  huyo alimnyonga mtoto, wakati mkewe akiwa nje ya nyumba akifua nguo.

Kwa mujibu wa kamanda, baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa alitoweka nyumbani na kwenda kusikojulikana.

Kamanda Paulo alisema jitihada za polisi kumsaka na kumkamata mtuhumiwa hazijazaa matunda, lakini zinaendelea.

Mama mzazi wa mtoto huyo Juliana, alisema alikuwa na ugomvi na mume wake uliotokana na madai  kwamba mtoto hakuwa wa kwake.

Alisema kauli hiyo ilikuja siku kadhaa baada ya yeye  kujifungua mtoto huyo.

 Kwa mujibu wa Juliana, mume wake alipotoka mahabusu, alimkuta na mimba ya miezi mitatu na kuanza kumshawishi, ili aitoe kwa madai kuwa haikuwa yake.

Alisema katika kipindi chote hicho, mume wake amekuwa akimtuhumu  kwamba hakuwa mwaminifu katika ndoa yao.

0 comments:

Chapisha Maoni